Codeblock Limited
Masharti ya matumizi
Masharti haya ni makubaliano kati yako na Codeblock Limited kuhusu kutumia Drafti Ligi: programu, tovuti hii, ukurasa wa kuongeza almasi na ukurasa wa akaunti yako. Kwa kufungua akaunti au kutumia Drafti Ligi unakubali masharti haya na Sera yetu ya faragha. Kama hukubaliani nayo, tafadhali usitumie Drafti Ligi.
1. Nani anaweza kucheza
- Lazima uwe na miaka 13 au zaidi.
- Kama una miaka 13 hadi 17, unahitaji ruhusa ya mzazi au mlezi kutumia Drafti Ligi na kufanya ununuzi, na wao wanawajibika kwa matumizi yako. Wachezaji walio chini ya miaka 18 wanapiga soga kwa maneno yaliyoandaliwa tu.
- Akaunti moja kwa kila mtu, kwa namba ya simu unayoimiliki. Usifungue akaunti kwa ajili ya wengine wala kutumia akaunti ya mtu mwingine.
2. Akaunti yako na usalama wake
- Unaingia kwa namba yako ya simu na msimbo wa mara moja tunaokutumia kwa SMS. Usimpe mtu yeyote msimbo wa kuingia. Hatutakuomba msimbo kamwe.
- Unawajibika kwa yanayotokea kwenye akaunti yako, kwa hiyo linda simu na laini yako. Ukipoteza simu au ukidhani mtu mwingine anatumia akaunti yako, tuandikie support@codeblock.co.tz mara moja.
- Kuhamishia akaunti kwenye namba mpya, wasiliana nasi; tunaweza kukuomba uthibitisho kuwa akaunti ni yako.
3. Mchezo wa haki
Shinda kwa akili yako mwenyewe. Hairuhusiwi:
- kutumia injini, roboti, mtu mwingine au msaada wowote wa nje ukicheza mechi ya daraja, ligi au mashindano;
- kuwa na akaunti zaidi ya moja, au kupoteza makusudi, ili kubadilisha viwango, msimamo au matokeo (pamoja na kupanga matokeo);
- kumfundisha mchezaji wakati wa mechi, kwa mfano kutoka kiti cha mtazamaji au soga nyingine;
- kutumia programu zilizobadilishwa, skripti au programu za kiotomatiki, au kutumia hitilafu (tafadhali ziripoti badala yake);
- kutumia vibaya kukatika kwa mtandao au saa ili usipoteze.
Tunatumia ukaguzi wa kiotomatiki na wa watu. Tukigundua udanganyifu tunaweza kufuta matokeo, kurekebisha viwango, kuondoa vyeo, beji na vitu vya bingwa, na kusimamisha au kufungia akaunti.
4. Soga na tabia
Soga ni ya kila mtu, kwa hiyo kuwa na heshima. Hakuna unyanyasaji, uonevu, matamshi ya chuki, vitisho, maudhui ya ngono, barua taka, utapeli wala matangazo, hakuna kutoa taarifa binafsi za mtu yeyote (namba za simu na viungo vinazuiwa), na hakuna kujifanya mfanyakazi wa Drafti Ligi.
Hatuvumilii kabisa maudhui yasiyofaa wala watumiaji wanaonyanyasa wengine: kwa kutumia Drafti Ligi unakubali kutoweka maudhui hayo wala kuwanyanyasa wachezaji wengine.
Tunachuja soga kiotomatiki na kushughulikia ripoti. Tunaweza kuficha ujumbe, kukunyamazisha kwenye chumba kimoja au kila mahali, au kusimamisha akaunti yako. Unaweza kuripoti na kumzuia mchezaji mwingine wakati wowote.
5. Vitu na sarafu za mchezo
Drafti Ligi ina sarafu mbili za mchezo: sarafu, unazozipata kwa kucheza, na almasi, unazoweza kununua. Unaweza kuzitumia kupata vitu vya mchezo kama mabao, vipande na viwanja.
- Hazina thamani ya pesa. Sarafu, almasi na vitu havina thamani ya kifedha. Haviwezi kubadilishwa kuwa pesa, kutolewa, kuuzwa, kubadilishana, kuhamishiwa akaunti nyingine wala kukombolewa kwa bidhaa halisi. Almasi si amana wala pesa za kielektroniki.
- Leseni, si umiliki. Unapopata sarafu, almasi au kitu, tunakupa leseni binafsi, isiyohamishika na inayoweza kubatilishwa ya kukitumia ndani ya Drafti Ligi. Huvimiliki.
- Ununuzi. Ununuzi ndani ya programu unapitia App Store au Google Play; kuongeza almasi kwenye tovuti kunalipwa kupitia ClickPesa. Bei inaonyeshwa kabla ya kulipa. Almasi zikishaingia, ununuzi umekamilika.
- Kurejeshewa pesa. Ununuzi ndani ya programu unarejeshwa kwa kanuni za Apple au Google: waombe wao. Kwa kuongeza almasi kwenye tovuti, wasiliana nasi kama malipo yalipita lakini almasi hazikuingia, au ulikatwa mara mbili, na tutaziweka almasi au kukurejeshea pesa. Hakuna chochote katika masharti haya kinachopunguza haki zako chini ya sheria ya Tanzania ya kumlinda mlaji.
- Malipo yaliyorudishwa. Malipo yakirejeshwa au kubatilishwa, tunaondoa almasi yaliyonunua. Salio lako linaweza kushuka chini ya sifuri, na duka linafungwa hadi lirudi sifuri au zaidi.
- Mabadiliko. Tunaweza kubadilisha bei, orodha ya vitu na jinsi sarafu zinavyopatikana. Baadhi ya vitu ni vya muda maalum. Tukiwahi kufunga Drafti Ligi, tutatoa taarifa ya angalau siku 30 ndani ya programu.
- Akaunti yako ikifutwa, au ikifungiwa kwa kuvunja masharti haya, sarafu, almasi na vitu vyake vinapotea, isipokuwa pale sheria inapotaka vinginevyo.
6. Hakuna zawadi na hakuna kamari
Drafti Ligi ni mchezo wa ujuzi unaochezwa kwa heshima tu. Kuingia kila ligi na mashindano ni bure, na hakuna anayeweka dau.
- Hatutoi zawadi za pesa wala vitu vyenye thamani ya pesa. Washindi wanapata vyeo, nafasi kwenye orodha na kwenye orodha ya heshima, na beji na vitu vya bingwa vinavyopatikana kwa kushinda tu, ambavyo havina thamani ya kifedha na haviwezi kuuzwa wala kuhamishwa.
- Hakuna kamari. Hairuhusiwi kuweka dau, au kupanga dau, kwenye mechi au matokeo ya Drafti Ligi, ndani au nje ya jukwaa. Akaunti zinazohusika na kamari zitafungiwa.
- Hatukubali wadhamini wa kamari au bahati nasibu.
7. Wadhamini
Baadhi ya ligi, mashindano, vitu na mabango yana jina na chapa ya mdhamini, na mashindano yaliyodhaminiwa yanatumia bao la mdhamini kwenye kila mechi (unabaki na vipande vyako). Wadhamini wananunua mwonekano tu: hawabadilishi sheria wala matokeo, na wanapokea ripoti za jumla tu, kamwe si taarifa zako binafsi. Wadhamini wanawajibika kwa maudhui na ofa zao.
8. Mkusanyiko wa Mashabiki
Mkusanyiko wa Mashabiki una skini halisi zilizochochewa na utamaduni wa mashabiki na rangi za majukwaa. Ni miundo iliyochochewa na mashabiki; haihusiani na, wala haijaidhinishwa na, klabu yoyote. Haitumii majina, nembo wala alama za biashara za klabu. Viwanja vimepewa majina ya mahali na havihusiani na klabu au uwanja wowote. Majina na alama za klabu ni mali ya wamiliki wake.
9. Maudhui yako
Unabaki na haki ulizonazo kwenye jina lako la kuonyesha na ujumbe wako wa soga. Unaipa Codeblock leseni ya dunia nzima, isiyo ya kipekee na bila malipo, ya kuvihifadhi, kuvionyesha, kuvinakili na kuvishiriki ndani ya Drafti Ligi na katika kuitangaza (kwa mfano mstari wa soga kwenye marudio, au klipu ya fainali), kwa muda unaohitajika kwa malengo hayo. Mechi na hatua zako zinaweza kuonyeshwa hadharani, kurudiwa na kutumika kwenye takwimu. Unawajibika kwa unachoandika.
10. Maudhui yetu
Programu, tovuti, michoro, skini na programu-tumizi, pamoja na jina Drafti Ligi, ni mali ya Codeblock au watoa leseni wake. Usivinakili, kuviuza, kuvichambua kinyume (reverse-engineer) wala kuvivuna kiotomatiki, wala kutengeneza programu zisizo rasmi, isipokuwa kama sheria inavyoruhusu.
11. Mabadiliko na upatikanaji
Tunaendelea kuboresha Drafti Ligi, kwa hiyo vipengele vinaweza kubadilika au kuondolewa. Unahitaji mtandao kucheza mtandaoni. Tunaweza kusimamisha huduma kwa matengenezo, na hatuwezi kuahidi kuwa itapatikana kila wakati au bila hitilafu.
12. Kusimamisha na kufunga akaunti
Unaweza kuacha kutumia Drafti Ligi wakati wowote na kufuta akaunti yako kwenye programu au kwenye drafti.co.tz/account. Tunaweza kusimamisha au kufunga akaunti inayovunja masharti haya, inayofanya ulaghai, inayohatarisha wachezaji wengine au pale sheria inapotaka, bila taarifa katika hali mbaya. Ukiona tumekosea, tuandikie support@codeblock.co.tz na tutalikagua upya.
13. Kanusho
Kwa kadiri sheria inavyoruhusu, Drafti Ligi inatolewa "kama ilivyo" na "kadiri inavyopatikana", bila ahadi kuwa itakidhi kila hitaji au itafanya kazi bila kukatika. Viwango na msimamo vinaweza kusahihishwa tukigundua kosa au udanganyifu.
14. Ukomo wa dhima
Kwa kadiri sheria ya Tanzania inavyoruhusu, Codeblock haiwajibiki kwa hasara isiyo ya moja kwa moja au inayofuata, faida au fursa zilizopotea, au kupotea kwa vitu vya mchezo, na dhima yetu yote kwako ina kikomo cha kiasi ulichotulipa katika miezi 12 kabla ya dai. Hakuna chochote katika masharti haya kinachoondoa dhima ambayo sheria haituruhusu kuiondoa, kama ya ulaghai, kifo au jeraha kutokana na uzembe, au haki zako kama mlaji.
15. Sheria inayotumika na migogoro
Masharti haya yanaongozwa na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ukiwa na malalamiko, tafadhali wasiliana nasi kwanza: matatizo mengi yanatatuliwa haraka kwa njia hiyo. Mgogoro wowote tusioweza kuumaliza utapelekwa kwenye mahakama zenye mamlaka za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
16. Mabadiliko ya masharti haya
Tunaweza kusasisha masharti haya. Tutabadilisha tarehe iliyo juu na, kwa mabadiliko muhimu, tutakujulisha ndani ya programu kabla hayajaanza kutumika. Ukiendelea kutumia Drafti Ligi baada ya hapo, masharti mapya yanatumika; usipokubali, unaweza kufuta akaunti yako.
Masharti haya yako kwa Kiswahili na Kiingereza.
17. Mawasiliano
Codeblock Limited. Barua pepe support@codeblock.co.tz, tovuti drafti.co.tz, msaada drafti.co.tz/support.